BIG 4 MILL

big4mill.blogspot.com.

Usisite kutembelea blog yako

Karibu nawe mahali popote... - big4mill.blogspot.com.

Tunaishi pamoja wakati wowote

http://www.big4mill.blogspot.com for more info - big4mill.blogspot.com.

Kazi zetu ni...

Tunaelimisha, kuburudisha na kadhalka.

Pata habari mbalimbali

Ndani na nje ya Tanzania/ kitaifa na Kimataifa - big4mill.blogspot.com.

Thursday 4 July 2013

FBI wakagua ofisi ya Kova kwa mbwa


 

. Ofisa mmoja wa Usalama wa Marekani (FBI), akiwa na mbwa jana aliingia Makao Makuu ya Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na kufanya ukaguzi.
Tukio hilo lilitokea muda mfupi kabla ya msafara wa magari ya Marekani kupita yakitokea Ikulu kwenda Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere kumlaki Rais Barack Obama.
Polisi ambaye hakutaka kutajwa alisema ofisa huyo  aliingia na mbwa hadi maeneo ya mapokezi, lakini muda mfupi walitoka.
“Walikwenda moja kwa moja mapokezi wakafanya ukaguzi,  kisha wakatoka nje ya jengo na kama hiyo haitoshi, ofisa huyo akiwa na mbwa alikwenda sehemu ya kuegesha magari yenye kesi na yale ya kawaida na kuanza kufanya ukaguzi, baada ya hapo waliondoka,” alisema polisi huyo na kuongeza:
“Licha ya mimi kutokuwa na  cheo pale, lakini hili la kutukagua na mbwa, ni kama wametudhalilisha... sisi ndiyo tunaaminika kwa usalama, leo hii wanatukagua na mbwa. Tena Kituo Kikuu.”
Hata hivyo, usalama kwenye vituo vingi ikiwamo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Juliusu Nyerere, vilikuwa chini ya usimamizi na uangalizi wa makachero wa Marekani.

Mandla: Mjukuu anayeinyima usingizi familia ya Mandela


Mjukuu wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Mandla Zwelivelile Mandel

Johannesburg. Mjukuu wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Mandla Zwelivelile Mandela ambaye ameibua mgogoro mkubwa katika familia ya shujaa huyo wa Afrika katika mzozo wa makaburi amekuwa na mlolongo wa visa katika maisha yake.
Visa hivyo kwa sehemu kubwa vinahusu maisha yake ya ndoa kwani ameoa na kuacha mara tatu huku akikabiliwa na kisa kingine cha kudaiwa kuuza haki za televisheni za kuonyesha mazishi ya Mzee Mandela.
Mandla ambaye jana aliamriwa na Mahakama kurejesha mabaki ya miili ya watoto watatu wa Mandela, alizaliwa mwaka 1974 na kwa sasa ni Chifu wa eneo la Mvezo. Ni msomi mwenye shahada ya kwanza ya siasa aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Rhodes mwaka 2007.
Chifu huyo wa Kabila la Xhosa amekuwa na vituko vingi katika maisha yake. Mwaka 2009 alizua utata baada ya kuuza haki ya kutangaza mazishi ya Mandela atakapokufa kwenye kituo cha televisheni cha SABC kwa Rand 3 milioni (Sh481 milioni).
Hata hivyo, suala hilo lilifikishwa katika Mahakama Kuu ya Mthatha ambako hukumu ilitoka na alipewa siku 15 kutangaza kama kweli ameuza haki ya matangazo ya mazishi ya Mandela au akanushe taarifa hizo.
Taarifa zilisema kuwa kutokana na shinikizo la baadhi ya wanafamilia na mkazo wa hukumu ya Mahakama, Mandla alilazimika kukanusha kuuza haki ya matangazo ya mazishi ya Mandela kwa kituo kimoja cha televisheni.
Mandla ambaye ni mtoto wa Makgatho Mandela aliyefariki dunia mwaka 2005 baada ya kuugua maradhi yanayofanana na ya Ukimwi, alipata hadhi ya uchifu baada ya kifo cha baba yake mwaka 2007.
Mandela ambaye alikabidhiwa uchifu wa uongozi wa watu wa Kabila la Xhosa takriban miaka 70, ndiye aliyempendekeza Mandla kuchukua wadhifa huo. Alikabidhiwa wadhifa huo mwaka 2007 wakati huo akiwa na umri wa miaka 32. Majukumu yake yalikuwa kuongoza sherehe za kimila, kutatua matatizo ya ndani ya ukoo wao na kuwakilisha Kabila la Xhosa katika masuala ya kisiasa.
Kutokana na majukumu hayo, Mandla alichaguliwa kuwa mbunge mwaka 2009 kupitia Chama cha African National Congress (ANC). Mke wake wa kwanza ni Tando Mabuna-Mandela aliyemuoa mwaka 2004. Hata hivyo, mwaka 2009, mwanamke huyo aliomba talaka mahakamani akidai kuwa mumewe huyo ni mgumba.
Mke wa pili wa Mandla ni Anais Grimaud aliyezaliwa mwaka 1990 huko Reunion ambaye alibadili jina lake na kuitwa Nkosikazi Nobubele. Walioana Machi 2010 katika ndoa ya kimila.
Septemba 2011 alipata mtoto aliyepewa jina la Qheya II Zanethemba Mandela na alikaribishwa kwa Mandela kijijini Qunu kwa taratibu za kimila. Hata hivyo, Agosti mwaka 2012, Mandla alimkataa mtoto huyo akidai mkewe alikuwa ana uhusiano na kaka yake, kesi ilifika mahakamani na waliachana kutokana na sababu hiyo.
Mkewe wa tatu ni Nodiyala Mbali Makhathini ambaye walioana Desemba 24, 2011, lakini tayari amefungua kesi ya kudai talaka.

Michelle Obama: Acheni kufuatilia mavazi yangu

“Watu wanapaswa kuelewa, wake za marais nao hufanya mambo mazuri ya jamii na kazi yao siyo kubadili staili za nywele na mavazi tu,” Michelle Obama
Dar es Salaam. Michelle Obama na Laura Bush walikuwa kivutio jana kwenye Mkutano wa wake wa marais wa Afrika unaoendelea Dar es Salaam, pale walipoongelea kwa mzaha jinsi vyombo vya habari vinavyoshupalia kuandika kuhusu staili za nywele na  mavazi ya wake wa marais, huku vikiacha masuala ya msingi.
Mkutano huo uliofunguliwa jana na Rais Jakaya Kikwete, ni maalumu kwa ajili ya kusaidia wanawake wajasiriamali wa Afrika, unatarajiwa kumalizika leo
.
Wakizungumza kwenye mjadala ulioongozwa na Mwandishi wa Habari wa Marerkani, Cokie Roberts,  Michelle, ambaye ni mke wa Rais wa Marekani, Barack Obama, alisema alifurahia kupata nafasi ya kufanya majadiliano na Laura, ambaye ni mke wa Rais wa zamani wa Marekani.
“Ninampenda mwanamke huyu,” alisema Michelle kwa utani kama vile hamfahamu.  
“Sishangai sana maana tuko klabu moja nadhani,”  alijibu Laura kwa utani akiwa na maana kuwa,  wao wote wana uzoefu wa kuwa wake wa marais.
“Unajua tunaishi maisha ya shida, maana wenzetu wa habari wanaangalia zaidi staili za mavazi na nywele zetu badala ya kuangalia mambo ya msingi,” alisema Michelle.

 

 Alisema mwanzoni mwa mwaka huu, alibadili staili ya nywele lakini alishangaa jinsi suala hilo lilivyokuzwa na vyombo vya habari.

Pinda aisaliti kauli yake, aruhusu tena sherehe


Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, 
Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amewaagiza Watanzania kuwa na uzalendo wa kuwaenzi na kuwakumbuka wenzao ambao wamefanya kazi  muda mrefu kwa kuthamini mchango wao.
Pinda alitoa kauli hiyo juzi katika viwanja vya Bunge, aliposhiriki hafla ya kuwaaga wafanyakazi waliostaafu utumishi na wale waliohamishwa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuanzia 2010.
Hata hivyo, Pinda alisema  yeye ndiye aliyemwagiza Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia kuandaa hafla hiyo ili kuwatunuku zawadi na kula nao chakula pamoja na watumishi hao, ambao idadi yao ilikuwa 59 kutoka sehemu mbalimbali nchini. Hata hivyo walihudhuria 35.
Juzi ilikuwa ni siku ya pili mfululizo kwa Pinda kushirikia warsha katika viwanja hivyo, siku iliyotangulia alikuwa ameshiriki  sherehe kubwa iliyoandaliwa na Bunge kumwaga Spika Mstaafu ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta ambaye alitumikia nafasi ya Uspika kwa miaka mitano 2005/10.
 Sherehe ya juzi ambayo iliandaliwa kwa agizo la Pinda, inapingana na kauli na maagizo yake ambayo amekuwa akitoa kwa nyakati tofauti kwamba, makongamano na warsha zisizo na tija ni ufujaji fedha za umma.
“Mimi ndiye niliyeamua kufanya hivi na huu ni ubinadamu tu nikaona nimtume mama Ghasia afanye maandalizi hayo, lengo kuu la hapa ni kukaa pamoja na wenzetu na kuwaambia kuwa tunashukuru kwa kazi yenu nzuri na pia tunathamini michango yenu,” alisema Pinda.
Alisema huo ulikuwa ni mwanzo, lakini Tamisemi itakuwa ikifanya hivyo kila mwaka  kuwaaga watu wanaostaafu na wanaohamia wizara zingine.
Kuhusu wastaafu hao, alisema Serikali inapaswa kuwathamini na kutambua michango yao wakati wote kuliko kuwatelekeza kama ilivyo sasa.
Alisema kustaafu kwa mtu sio kwamba anakuwa amepungukiwa hekima na maarifa, bali ni utaratibu ukifika wakati fulani anatakiwa kupumzika.
Licha ya hilo,  aliwaagiza viongozi wa Tamisemi kuangalia uwezekano wa kuwasaidia watu wanaojiandaa kustaafu ili wajenge nyumba za kufikia na familia zao, kwani wengine humaliza muda  na kushindwa  kujenga. 
Tangu kuingia ateuliwe, Pinda amekuwa akipiga vita sherehe na ununuzi wa magari ya kifahari kwa madai kuwa, ni ubadhirifu wa fedha za umma.
Hatua hiyo inaonyesha ameanza kubariki fedha hizo kufanya sherehe.

My Blog List