Dar. Msanii wa muziki wa miondoko ya R’n’B,
Benard Paul maarufu kama Ben Pol wiki hii anatarajia kuachia video ya
wimbo wake mpya unaoitwa Jikubali ambao ameutoa wiki iliyopita .
Mbali na hilo, Ben Pol ameeleza kuwa siri ya yeye
kuingia kwenye vipengele vitano katika tuzo muziki za Kilimanjaro mwaka
huu ni kutokana na kazi nzuri anazozifanya ambazo mashabiki wanazikubali
na hakuna kingine hivyo alistahili
Aliliambia Mwananchi mwisho wa wiki kuwa mwaka huu
umekuwa wenye mafanikio kwake, kwani toka aanze muziki hakutarajia kama
ipo siku ataangiza nyimbo kwenye vipengele vingi.
“Mwaka juzi (2011) niliingiza wimbo mmoja na mwaka
jana nyimbo mbili, hapo utaona jinsi gani ninavyopiga hatua kutoka
kwenye nyimbo hizo hadi kufikia kuingiza nyimbo tano mwaka huu.
Kwa hakika hili ni jambo la kujivunia , nawashukuru Watanzania kwa msaada wao,” anasema.
Katika hatua nyingine, msanii huyoamewaomba
Watanzania wasisite kumpigia kura kwenye kinyang’nyiro hicho ili aweze
kunyakuwa tuzo hizo mwaka huu na hatimaye aweke historia ya kuwa msanii
wa kwanza wa RnB kunyakua tuzo nyingi.