Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
Dodoma. Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amewaagiza
Watanzania kuwa na uzalendo wa kuwaenzi na kuwakumbuka wenzao ambao
wamefanya kazi muda mrefu kwa kuthamini mchango wao.
Pinda alitoa kauli hiyo juzi katika viwanja vya
Bunge, aliposhiriki hafla ya kuwaaga wafanyakazi waliostaafu utumishi na
wale waliohamishwa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuanzia 2010.
Hata hivyo, Pinda alisema yeye ndiye aliyemwagiza
Waziri wa Tamisemi, Hawa Ghasia kuandaa hafla hiyo ili kuwatunuku
zawadi na kula nao chakula pamoja na watumishi hao, ambao idadi yao
ilikuwa 59 kutoka sehemu mbalimbali nchini. Hata hivyo walihudhuria 35.
Juzi ilikuwa ni siku ya pili mfululizo kwa Pinda
kushirikia warsha katika viwanja hivyo, siku iliyotangulia alikuwa
ameshiriki sherehe kubwa iliyoandaliwa na Bunge kumwaga Spika Mstaafu
ambaye pia ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta
ambaye alitumikia nafasi ya Uspika kwa miaka mitano 2005/10.
Sherehe ya juzi ambayo iliandaliwa kwa agizo la
Pinda, inapingana na kauli na maagizo yake ambayo amekuwa akitoa kwa
nyakati tofauti kwamba, makongamano na warsha zisizo na tija ni ufujaji
fedha za umma.
“Mimi ndiye niliyeamua kufanya hivi na huu ni
ubinadamu tu nikaona nimtume mama Ghasia afanye maandalizi hayo, lengo
kuu la hapa ni kukaa pamoja na wenzetu na kuwaambia kuwa tunashukuru kwa
kazi yenu nzuri na pia tunathamini michango yenu,” alisema Pinda.
Alisema huo ulikuwa ni mwanzo, lakini Tamisemi
itakuwa ikifanya hivyo kila mwaka kuwaaga watu wanaostaafu na
wanaohamia wizara zingine.
Kuhusu wastaafu hao, alisema Serikali inapaswa
kuwathamini na kutambua michango yao wakati wote kuliko kuwatelekeza
kama ilivyo sasa.
Alisema kustaafu kwa mtu sio kwamba anakuwa
amepungukiwa hekima na maarifa, bali ni utaratibu ukifika wakati fulani
anatakiwa kupumzika.
Licha ya hilo, aliwaagiza viongozi wa Tamisemi
kuangalia uwezekano wa kuwasaidia watu wanaojiandaa kustaafu ili wajenge
nyumba za kufikia na familia zao, kwani wengine humaliza muda na
kushindwa kujenga.
Tangu kuingia ateuliwe, Pinda amekuwa akipiga vita
sherehe na ununuzi wa magari ya kifahari kwa madai kuwa, ni ubadhirifu
wa fedha za umma.
Hatua hiyo inaonyesha ameanza kubariki fedha hizo kufanya sherehe.