Mjukuu wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, Mandla Zwelivelile Mandel
Johannesburg. Mjukuu wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson
Mandela, Mandla Zwelivelile Mandela ambaye ameibua mgogoro mkubwa katika
familia ya shujaa huyo wa Afrika katika mzozo wa makaburi amekuwa na
mlolongo wa visa katika maisha yake.
Visa hivyo kwa sehemu kubwa vinahusu maisha yake
ya ndoa kwani ameoa na kuacha mara tatu huku akikabiliwa na kisa kingine
cha kudaiwa kuuza haki za televisheni za kuonyesha mazishi ya Mzee
Mandela.
Mandla ambaye jana aliamriwa na Mahakama kurejesha
mabaki ya miili ya watoto watatu wa Mandela, alizaliwa mwaka 1974 na
kwa sasa ni Chifu wa eneo la Mvezo. Ni msomi mwenye shahada ya kwanza ya
siasa aliyoipata katika Chuo Kikuu cha Rhodes mwaka 2007.
Chifu huyo wa Kabila la Xhosa amekuwa na vituko
vingi katika maisha yake. Mwaka 2009 alizua utata baada ya kuuza haki ya
kutangaza mazishi ya Mandela atakapokufa kwenye kituo cha televisheni
cha SABC kwa Rand 3 milioni (Sh481 milioni).
Hata hivyo, suala hilo lilifikishwa katika
Mahakama Kuu ya Mthatha ambako hukumu ilitoka na alipewa siku 15
kutangaza kama kweli ameuza haki ya matangazo ya mazishi ya Mandela au
akanushe taarifa hizo.
Taarifa zilisema kuwa kutokana na shinikizo la
baadhi ya wanafamilia na mkazo wa hukumu ya Mahakama, Mandla alilazimika
kukanusha kuuza haki ya matangazo ya mazishi ya Mandela kwa kituo
kimoja cha televisheni.
Mandla ambaye ni mtoto wa Makgatho Mandela
aliyefariki dunia mwaka 2005 baada ya kuugua maradhi yanayofanana na ya
Ukimwi, alipata hadhi ya uchifu baada ya kifo cha baba yake mwaka 2007.
Mandela ambaye alikabidhiwa uchifu wa uongozi wa
watu wa Kabila la Xhosa takriban miaka 70, ndiye aliyempendekeza Mandla
kuchukua wadhifa huo. Alikabidhiwa wadhifa huo mwaka 2007 wakati huo
akiwa na umri wa miaka 32. Majukumu yake yalikuwa kuongoza sherehe za
kimila, kutatua matatizo ya ndani ya ukoo wao na kuwakilisha Kabila la
Xhosa katika masuala ya kisiasa.
Kutokana na majukumu hayo, Mandla alichaguliwa
kuwa mbunge mwaka 2009 kupitia Chama cha African National Congress
(ANC). Mke wake wa kwanza ni Tando Mabuna-Mandela aliyemuoa mwaka 2004.
Hata hivyo, mwaka 2009, mwanamke huyo aliomba talaka mahakamani akidai
kuwa mumewe huyo ni mgumba.
Mke wa pili wa Mandla ni Anais Grimaud aliyezaliwa
mwaka 1990 huko Reunion ambaye alibadili jina lake na kuitwa Nkosikazi
Nobubele. Walioana Machi 2010 katika ndoa ya kimila.
Septemba 2011 alipata mtoto aliyepewa jina la
Qheya II Zanethemba Mandela na alikaribishwa kwa Mandela kijijini Qunu
kwa taratibu za kimila. Hata hivyo, Agosti mwaka 2012, Mandla alimkataa
mtoto huyo akidai mkewe alikuwa ana uhusiano na kaka yake, kesi ilifika
mahakamani na waliachana kutokana na sababu hiyo.
Mkewe wa tatu ni Nodiyala Mbali Makhathini ambaye walioana Desemba 24, 2011, lakini tayari amefungua kesi ya kudai talaka.
0 comments:
Post a Comment