Kagasheki, Lembeli wapingana kwa takwimu
Kwa ufupi
- Taarifa za Serikali kuwa tembo 10,000 wanauawa kila mwaka si sahihi kwa kuwa zimeandaliwa na maofisa wa Serikali kwa ajili ya kuwatetea.
Iringa. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Ardhi, Maliasili na Utalii, James Lembeli amepinga kauli zilizotolewa
na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki kuhusu tembo
wanaouawa nchini kutokana na ujangili.
Waziri Kagasheki alisema kuwa kwa mujibu wa
utafiti uliofanywa na Tawiri, zaidi ya tembo 10,000 huuawa kila mwaka na
majangili kitu ambacho kinatishia maisha ya wanyama hao hapa nchini.
Kagasheki alisema hayo alipokuwa akifungua mkutano
wa Waandishi wa habari wa Vyombo vya Habari nchini na Shirika la
Hifadhi za Taifa(Tanapa) uliofanyika Iringa jana.
Hata hivyo Lembeli alisema kiasi kilichosemwa na
Waziri ni kidogo kwa kuwa watafiti waliotoa takwimu hizi ni wa Serikali
hivyo wanaficha baadhi ya mambo.
“Taarifa za Serikali kuwa tembo 10,000 wanauawa
kila mwaka si sahihi kwa kuwa zimeandaliwa na maofisa wa Serikali kwa
ajili ya kuwatetea,” alisema Lembeli.
Alisema tatizo la ujangili wa meno ya tembo nchini
ni kubwa na idadi inayotolewa ni kwa wale tembo wanaouawa kwenye
hifadhi tu wakati wengi bado wanauawa na majangili nje ya hifadhi za
Taifa.
Aidha aliwataka wanahabari kutokuwa waoga katika
kufichua habari za majangili wa meno ya tembo kwa kuwa wanaojihusisha na
meno ni watu wenye uwezo mkubwa kifedha na wana mitandao mikubwa.
“Ni vyema wanahabari kutokuwa waoga katika
kufichua mitandao ya ujangili kwa kuwa wanaohusika wana fedha na kuna
viongozi ambao wanawaunga mkono”, alisema Lembeli.
Akizungumzia umuhimu wa vyombo vya habari
Kagasheki alivitaka kuisaidia Serikali kukabiliana na vita dhidi ya
ujangili wa tembo na wanyamapori wengine.
Aliwaomba waandishi wa habari kusaidia kwa kuwa
kuna rushwa bandarini, viwanja vya ndege, ndani ya Mahakama, serikalini,
polisi, idara ya usalama, na mamlaka ya mapato ndiyo maana ujangili
hasa wa meno ya tembo unaongezeka.
Alisema watalii havutii kuwaona tembo wanaoendelea kupungua duniani kote kutoka milioni 50 mwaka 1930 hadi 402,067 mwaka jana.
Kagasheki alisema kwa upande wa Tanzania idadi
yake imepungua kutoka kati ya tembo 250,000 na 300,000 katika miaka ya
sitini hadi hadi 110,000 mwaka 2009
0 comments:
Post a Comment