Marekani yataja sababu nne za Obama kuja Tz
- Alisema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano linapokuja suala la uongozi bora na ndiyo maana imekuwa na amani na utulivu kwa muda mrefu ikilinganishwa na nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Dar es Salaam. Marekani imetaja sababu nne
ambazo zimemfanya Rais Barrack Obama kuijumuisha Tanzania katika ziara
yake ya bara la Afrika.
Rais Obama amepanga kulitembelea bara la Afrika
kuanzia Juni 26 hadi Julai 3, mwaka huu na atazitembelea pia Senegal na
Afrika Kusini.
Kiongozi huyo wa Marekani ambaye baba yake mzazi
ni mzaliwa wa Kenya, anatarajiwa kuwasili nchini Julai Mosi kwa ziara ya
siku tatu. Atakuwa Rais wa tatu wa Marekani kuitembelea Tanzania baada
ya Bill Clinton mwaka 2000 na George Bush mwaka 2008.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
jana, Balozi wa Marekani, Alfonso Lenhardt alisema sababu ya kwanza ya
Obama kuja Tanzania ni kutokana na kuwa mfano wa utawala bora,
demokrasia na ushirikishaji wa watu wake wakati wa kufanya uamuzi
unaogusa maisha yao ya kila siku.
Alisema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano linapokuja
suala la uongozi bora na ndiyo maana imekuwa na amani na utulivu kwa
muda mrefu ikilinganishwa na nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
“Nchi nyingi za Afrika zinazoizunguka Tanzania
zimekuwa na matatizo ya vita vya wenyewe na hata ukosefu wa utawala
bora,” alisema Balozi Lenhardt ingawa alidokeza kuwa katika siku za
karibuni imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali kutokana na
matukio ya uvunjifu wa amani.
Balozi Lenhardt alisema sababu nyingine
inayomfanya Rais Obama kuja Tanzania ni kutokana na jitihada za Serikali
ya Marekani kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji na kasi ya ukuaji
wa uchumi.
“Rais Obama anakuja kuunga mkono juhudi za
Watanzania katika kutengeneza mazuri ya uwekezaji lakini bila kusahau
kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania imeivutia Serikali ya
Marekani,” alisema.
Balozi Lenhardt alitaja sababu nyingine inayomleta
Rais Obama kuwa ni kuisaidia Tanzania kuendeleza fursa mbalimbali za
kujiletea maendeleo.
Alisema uendelezaji huo wa fursa una lengo la kuisaidia Serikali ya Tanzania kukabiliana na tatizo la umaskini.
Alisema Marekani ni moja ya nchi zinazoongoza kwa
kutoa fedha nyingi za misaada na akisema kwa mfano, mwaka 2012 pekee
ilitoa Dola 750 milioni.
Aidha, alisema nchi yake imekuwa ikitoa misaada
mingi kupitia Shirika la Millenium Challenge (MCC), ambayo imejikita
zaidi katika kusaidia sekta za umeme, maji na miundombinu.
0 comments:
Post a Comment